Posted by:HABARI LEO
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeamuru shehena ya mafuta ya
petroli iliyoagizwa kutoka Falme za Kiarabu irejeshwe ilikotoka kutokana
na kubaini hayana ubora unaotakiwa kwa matumizi ya magari na mitambo.
Akitoa taarifa hiyo Dar es Salam jana, Mkurugenzi Mkuu wa shirika
hilo, Joseph Masikitiko alisema, vipimo vya maabara vya sampuli ya
mafuta hayo vimeonesha kuwa hayafai kwa matumizi. Alisema hayo ni matokeo ya ukaguzi wa hivi karibuni wa shehena hiyo
yenye ujazo wa tani za metriki 38,521.018 katika meli ya MT. Ridgebury
John B, yaliyokuwa yasambazwe na kuuzwa nchini.
Alisema, "Vipimo vinaonesha kuwa baadhi ya matakwa ya viwango vya
mafuta ya petroli hayajafikiwa, hivyo kuamuru yarejeshwe yalikotoka.
Kiwango cha ubora cha mafuta ya petroli ni TZS 672:2012/ EAS 158:2012
ambacho hakikufikiwa".
Matakwa ya kiwango ambacho mafuta hayo hayakukidhi ni pamoja na kuwa
na kemikali zilizo na oksijeni ndani yake ambazo husababisha madhara
kwenye injini za magari na mitambo.Alisema, "Kiwango cha petroli hakiruhusu uwepo wa kemikali hizo
kwenye mafuta hayo kwa sababu zinaua injini, kuhatarisha afya za watu na
kuharibu mazingira kutokana na kusababisha moshi mchafu mwingi".
Alifafanua kuwa mafuta hayo yameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa
kuvuta maji au mvuke na kuwa sehemu ya petroli, kiasi cha kuifanya iwe
na maji mengi ambayo ni hatari kwa injini za magari na mitambo.
Pia, alieleza uhafifu mwingine katika mafuta hayo kuwa ni kupungua
kwa nguvu ya kuendesha injini au mitambo hivyo kusababisha uharibifu na
hasara. Aliongeza kuwa, mvuke unapokuwa mwingi kwenye petroli
husababisha mtiririko wa mafuta kwenda kwenye injini kutokuwa mzuri,
huku kemikali aina ya benzene iliyoonekana kuzidi katika petroli hiyo
ikiwa ni chanzo cha kansa kwa wanaotoa huduma ya uuzaji wa mafuta hayo.
Sambamba
na hayo, Masikitiko aliongeza kuwa walibaini kuwa uhafifu
katika mafuta hayo unaongeza wingi wa ujazo wa nishati hiyo pasipokuwa
na uhalisia na kisha kutoa nguvu isiyolingana na wingi wake. Alisema,
madhara yake ni mnunuzi kulipia wingi wa mafuta usio na thamani
halisi.Aliwahakikishia watumiaji wa mafuta kuwa, shirika hilo
litahakikisha
linafanya ukaguzi katika meli zote zenye mafuta yanayokusudiwa
kusambazwa nchini ili kuzuia yasiyo na ubora yasiingizwe sokoni.
Katika hatua nyingine, Tbs ilisema kuwa iliagiza vilainishi vya
mitambo na magari vya kampuni ya HASS Petroleum (T) Limited vyenye ujazo
wa lita 16,080 kutoka Falme za Kiarabu virejeshwe vilikotoka pia kwa
sababu ya kukosa ubora unaofaa kwa matumizi na kwamba mwagizaji
alitekeleza agizo hilo tangu Desemba 31 mwaka jana.
Ewura yazungumza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA)
imekiri kufahamu kuhusu suala hilo na kueleza wananchi kuwa licha ya
mafuta hayo kutakiwa kurejeshwa yalipotoka, bado nchi ina akiba ya
petroli inayoweza kutumika hadi shehena nyingine iletwe."Wananchi wasiwe na wasiwasi," alisema Mkuu wa Idara ya Mawasiliano
wa Ewura, Titus Kaguo. Alisema kwa siku nchi inatumia lita za petroli
2,700,000, na kwamba kila metriki tani moja ya petroli huwa na lita
700,000.
"Kwa maana hiyo, lita 33,000,000 za petroli zilizokuja na kukataliwa
endapo zingeshushwa na kutumika nchini zingeweza kutosheleza mahitaji
kwa zaidi ya siku saba," alisema Kaguo . Hata hivyo, aliongeza kuwa si
mafuta yote yanayoingia na meli bandarini hushushwa kwa ajili ya
matumizi ya nchi, bali mengine huwa safarini kwenda nchi nyingine.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu dompromo92@gmail.com au Whatsapp namba +255759399445.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu dompromo92@gmail.com au Whatsapp namba +255759399445.
0 comments:
Post a Comment